Na Seif Shaggy Gracien Hasingizwimana/Kigali,Rwanda,
Msanii wa kike Zuchu kutoka Tanzania, ambaye hivi karibuni alicheza na hisia za mashabiki wake, anaendelea kuwa gumzo kuu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuweka picha zake zinazomwonyesha akiwa mjamzito.
Katika siku zilizopita, msanii huyu ambaye hivi karibuni alitangaza kuwa wametengana na Diamond Platnumz, kwa sasa amewashangaza wengi kwa picha alizoweka kwenye Instagram yake zinazomwonyesha akiwa amevaa nguo zilizomshika mwili, tumbo likionekana wazi, na akionekana kama yuko kwenye maandalizi ya kupokea mtoto katika mfumo unaojulikana kama “baby shower”.
Picha hizi zilizua sintofahamu kubwa kwa mashabiki wake, kutokana na kwamba katika siku zilizopita alikuwa amekanusha taarifa zilizosema kuwa huenda ni mjamzito au alishajifungua. Zuchu wakati huo alisema kuwa taarifa hizo hazijui na kwamba ni uvumi uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kuonekana kwa picha hizi kunatokea baada ya hivi karibuni kutangaza kuwa ametengana na msanii Diamond Platnumz, ambapo alisema kuwa wote wawili walichagua kutengana baada ya miaka yapata sita waliyokuwa wamekaa kwenye mahusiano ya kimapenzi, akisema kuwa kila mmoja anaenda kuangazia maisha yake na kuendelea kufanya muziki wake.

Mbali na masuala ya mapenzi yake na Diamond, miongoni mwa mambo mengine yanayoendelea kuibua mijadala kati ya watu ni kwamba kwenye Instagram ya Zuchu haionekani tena kama bado anafanya kazi na lebo ya Wasafi ya Diamond Platnumz.
Zuchu aliingia kwenye muziki mnamo mwaka 2020 akisainiwa na WCB Wasafi, na mara moja akaonyesha uwezo wake kama mmoja wa wasanii wa kike wakubwa zaidi katika Afrika Mashariki.
Msanii Zuchu alisikika sana kwenye nyimbo mbalimbali alizoshirikiana na Diamond Platnumz, zikiwemo Inama, Mtasubiri, Wale Wale, na Raha pamoja na zingine.






