Jumamosi, Agosti 8, 2026
spot_imgspot_img

Top 5 This Week

spot_img

Related Posts

Maafisa Ugani 311 Wapewa Vyeti, Wanatarajiwa Kuongeza Uzalishaji wa Wakulima

Na Seif Shaggy Gracien Hasingizwimana/Kigali,Rwanda,

Maafisa ugani 311 wamekamilisha mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo na Mifugo (MINAGRI) kupitia Taasisi ya Kitaifa ya Kuendeleza Kilimo na Mifugo (RAB), kwa ushirikiano na One Acre Fund.

Maafisa ugani hao walipewa vyeti vinavyotambulika kitaifa, baada ya kufunzwa kuhusu kilimo cha kisasa, kuhifadhi udongo, na kutumia mbinu zinazoweza kuongeza uzalishaji.

Miongoni mwao, kuna washauri wa kilimo 234 wanaofanya kazi kwenye vitalu vya mbegu (byanya bigega) pamoja na wafanyakazi 77 wa One Acre Fund wanaohusika na ufuatiliaji wa shughuli za shirika hili sehemu mbalimbali nchini.

Miongoni mwa mambo waliyotakiwa kutekeleza ni pamoja na kuwa karibu na wakulima, kuwashauri, na kuwasaidia kulima kwa njia za kisasa, ili wapate mazao mengi na yenye ubora.

Mukeshimana Drocella, anayehusika na ugani katika Sekta ya Kivuye, Wilaya ya Burera, alisema kuwa ujuzi waliopata utawasaidia kuwasaidia wakulima kulima kwa njia za kisasa.

Alisema: “Tunaenda kuwasaidia wakulima kulima kwa njia za kisasa, ili wapate mazao mengi na yenye ubora, ili waweze kujitosheleza kwa chakula na kupata vya kupeleka sokoni.”

Alisema pia kuwa katika mafunzo hayo walipata ujuzi wa jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, na kumsaidia mkulima kutoka kwenye kilimo cha kujikimu tu na kuingia kwenye kilimo cha kibiashara/kitaalamu.

Dushimiyimana Eric, mmoja wa waliohitimu mafunzo hayo, aliwaomba wasimamizi wa kilimo kuwa karibu na wakulima, wasikilize changamoto zao na kile wanachotamani kufanyiwa.

Alisema kuwa mafunzo hayo yaliwasaidia kuona mbinu za kuboresha kilimo, hasa katika maeneo ambayo kilimo hakikuwa kikifanyika kwa njia za kisasa.

Alisema: “Mchango wetu ni kusaidia kuinua kilimo ambacho kilikuwa hakiko vizuri. Kuna mahali ambapo kilimo hakikuwa kikifanyika kwa njia za kisasa, lakini tangu tuanze mafunzo haya kuna mabadiliko yameanza kuonekana. Tunaenda kuendelea kuwafundisha wakulima.”

Dushimiyimana alisema pia kuwa wanaenda kuweka juhudi katika kuhifadhi udongo, hasa katika kukabiliana na mmomonyoko wa udongo.

Alisema: “Kukabili mmomonyoko wa udongo ilikuwa moja ya changamoto kubwa zilizoonekana, lakini sasa tunaenda kuweka juhudi katika kuhifadhi udongo ili usibaki tena wazi.”

Alitoa mfano wa baadhi ya wakulima walioongeza uzalishaji wa viazi mbalimbali kutoka tani tano au kumi kwa hektari hadi kufikia tani 20 na 25, baada ya kufuata mbinu za kisasa walizofundishwa.

Sonia Muhikaze, Mkurugenzi Mkuu anayehusika na uratibu wa shughuli za One Acre Fund na Serikali ya Rwanda, alisema kuwa ushirikiano wa shirika hili na Serikali umesaidia zaidi ya wakulima milioni mbili kupata ujuzi na msaada katika kilimo.

Muhikaze alisema kuwa tangu mwaka 2015, shughuli za ugani zimeongezeka kwa 400%, na kwamba mbinu hii imechangia katika utekelezaji wa sera za nchi za ugani na kutoa taarifa zinazosaidia kufanya maamuzi yanayoongeza uzalishaji.

Alisema pia kuwa waliohitimu awamu ya kwanza ya mafunzo haya walichangia katika kuongeza uzalishaji wa kilimo kwa kiwango cha 16% kupitia matumizi ya pembejeo na kuhifadhi udongo.

Vyeti hivyo vilitolewa katika sherehe za kufunga Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mifugo ya 19 yaliyofanyika Mulindi, Mjini Kigali, yaliyohudhuriwa na waonyeshaji zaidi ya 670.

Waziri wa Kilimo na Mifugo, Dr Telesphore Ndabamenye, alisema kuwa Serikali ya Rwanda itaendelea kuwaunga mkono wakulima ili kile wanachofanya kilete faida zaidi.

Alihamasisha wakulima, wafugaji na wadau wengine kutumia ujuzi waliopata, hasa kuanzia msimu wa kilimo wa Septemba 2026.

Alisema: “Uzalishaji utapimwa kwa kasi ya mabadiliko ya kilimo na mifugo, pamoja na jinsi vitakavyochangia katika kuongeza uzalishaji na kuendeleza nchi kwa ujumla.”

One Acre Fund inayojulikana kama Tubura ina lengo la kufikia vitalu vya mbegu (byanya bigega) 1,100 na kusaidia wakulima zaidi ya elfu 115 wanaolima kwenye zaidi ya hektari elfu 62 isipitapo mwaka 2030.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Popular Articles