Na Seif Gracien Hasingizwimana/Kigali,Rwanda,
Katika Wilaya ya Huye, 53% ya wanawake wanaojishughulisha na kilimo wamepewa zana za kumwagilia maji kupitia mradi wa Sustainable Agricultural Intensification and Food Security Project (SAIP II), kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuinua hali yao ya maisha.
SAIP II inafadhiliwa na Global Agriculture and Food Security Program (GAFSP) kupitia Benki ya Dunia, na inatekelezwa na Taasisi ya Rwanda ya Utafiti na Maendeleo ya Kilimo na Mifugo (RAB), kupitia Kitengo cha Utekelezaji wa Mradi Mmoja (RAB-SPIU).
Katika Wilaya ya Huye, wananchi wanatarajia kupata zaidi ya hekta 20 za kulima, huku hekta nyingine 50 zikiwa tayari zimeshisaidiwa na mradi huu katika mbinu za kilimo bora na kumwagilia maji, ili wakulima waweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Sebutege Ange, Meya wa Wilaya ya Huye, anasema kuwa wananchi hawapaswi kulima kwa kutegemea tu kile hali ya hewa ilivyopanga, bali wakulima wanapaswa kulima kwa kumwagilia maji ili kuongeza uzalishaji wao.

Alisema: “Hii lazima iendane na kupata uwezo wa zana wanazopewa, kuwe na mafunzo na kuunganishwa na masoko, ili uzalishaji uliopatikana uweze kufika sokoni, ukiwa ni mfumo wa kilimo unaolenga kuongeza uzalishaji.”
Sebutege anaendelea kusema kuwa wanafurahia hatua waliyofikia, kwani wananchi wenyewe wanaishukuru na kushiriki katika shughuli zinazolenga kuongeza mafanikio endelevu, zitakazowasaidia kujitosheleza kwa chakula.
Alisema: “Tunashukuru hatua tuliyofikia, kwa sababu wananchi wenyewe wanaithamini na kuifanya kuwa yao ili idumu na kutusaidia kujitosheleza kwa chakula, kwani hiyo ndiyo agenda ya nchi yetu sote.”
Meya wa Wilaya ya Huye anasema kuwa kwa ushirikiano na SAIP II, kwanza zilisaidiwa vyama vya Ushirika vinavyofanya kazi mabondeni katika kuzuia mmomonyoko wa udongo, kwani ungejiri ungeharibu kile walichokifikia.
Anasema kuwa wakati wa kiangazi, maji hayakufika kwa kiasi cha kutosha maeneo ya milimani, hivyo wananchi walioko pembezoni mwa mabonde wakapewa zana za kuwasaidia kumwagilia maji na kuendelea kulima vyema kwa njia inayolinda udongo usimomonyoke.

Alisema: “Kwa ushirikiano na mradi wa SAIP II, wakati wa kiangazi mvua hainyeshi eneo la milimani na maji hayafiki kwa kiasi cha kutosha. Sasa nao wamepewa zana za kuwasaidia kumwagilia ili wananchi walioko pembezoni mwa mabonde waweze kulima vyema kwa njia inayotunza udongo, na pia kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia ya kumwagilia kwa zana walizopewa na mradi wa SAIP II, na pia kuwasaidia kupata mahali pa kuhifadhia mazao kabla hayajafikishwa sokoni.”
Mchango wa SAIP II Katika Kumwagilia Maji
Meya wa Wilaya ya Huye anasema kuwa karibu 85% ya wakulima wa wilaya hiyo wana chini ya hekta 0.5.
Alisema: “Inaeleweka kuwa tunapoweza kuunganisha karibu hekta 50 ni njia ya kuongeza uzalishaji na wakati huo wakalima msimu yote mitatu, jambo linalotusaidia kufikia lengo la kujitosheleza kwa chakula.”
Anaendelea kusema kuwa Wilaya ya Huye na wadau wameomba miradi kama SAIP II isaidie wakulima wenye maeneo madogo kuwa na uwezo wa kumwagilia maji na kulima katika majira yote matatu.
Meya Sebutege Ange anavishauri vyama vya ushirika na wakulima binafsi waliopewa zana za kumwagilia maji kuzitumia vyema na kuzitunza ili zisiharibike.
Alisema: “Kati ya mambo ninayowaambia wakulima au wadau ni kwamba fursa haitokei mara mbili, lakini shughuli zinazofanyika zinatokana na mahitaji waliyoomba ili kuongeza uzalishaji. Tunachowaomba ni kwamba zana walizopewa wazitumie kuzalisha na wajaribu kuzitunza, huku wakifanya mipango ya kutosha, kwa sababu tukiwa msimu wa mvua tunasema maji yanakuwa mengi na wakati mwingine yanatuharibia.”
Katika kutafuta majawabu, Meya wa Wilaya ya Huye anasema wakulima wanapaswa kuchimba madimbwi yanayoweza kuwasaidia kukusanya maji, ili zana walizopewa zitumike kwa kilichokusudiwa.
Alisema: “Hasa wakati wananchi wanaposubiri kuzitumia tu kwa maji yanayotoka mabondeni au mitoni, hata wakati wa kiangazi kali tunajua kuna miti inayoweza kukauka katika maeneo mbalimbali. Hivyo wakulima wanatakiwa kufanya mipango kulingana na kile hali ya hewa ilivyotoa, ili waweze kujiwekea akiba, kwa njia itakayowasaidia kuongeza uzalishaji wa kile walichopewa.”
Meya Ange anasema pia kuwa bidhaa za mafuta bado ni miongoni mwa changamoto zinazowasumbua wakulima, lakini wanafurhia kwamba wanaendelea kupewa zana zinazotumia nishati ya jua.
Alisema: “Tukishirikiana na mradi wa SAIP II, kinachowasumbua wakulima wengi ni bidhaa za mafuta, lakini pia tunashukuru kwamba wanaendelea kupewa na zinazotumia nishati ya jua, tukiamini kuwa wanaweza kuzitumia kuzalisha bila kukumbana na vikwazo, na kufanya kazi katika vikundi kuwasaidia kufanya kazi kwa umoja.”
Wanawake na Vijana Katika Shughuli za SAIP II
Katika Wilaya ya Huye, idadi kubwa ya wananchi wanaojishughulisha na kilimo ni wanawake ambapo katika Chama cha Ushirika cha Ruhashya, wanawake ni 53%, maana yake zana wanazopewa zinawafikia wote na kuwasaidia kujitunza. Wanawake pia wanashirikiana na vijana ili nao wasiachwe nyuma.

Meya Sebutege Ange anasema kuwa mafunzo mengi yanayotolewa na SAIP II katika kuwajengea uwezo wakulima yanawajumuisha na vijana.
Alisema: “Mafunzo mengi yanayotolewa na SAIP II katika kuwajengea uwezo wakulima, vijana pia wamo ndani yake, kwa sababu kuna vitalu vya miche vilivyotengenezwa wakulima bakapewa miti ya matunda na tunashirikiana na vyama vya ushirika vinavyoindaa ili vifanywe na vijana, nao waingie katika shughuli za kilimo, kwa sababu ni kazi inayoweza kuwaendeleza ikifanywa vyema na kwa kuipa muda wako.”
SAIP II Inyanyua Uzalishaji wa Chama cha Ushirika cha Terimbere
Mazimpaka Saveri, Rais wa Chama cha Ushirika cha Terimbere kinachofanya kazi katika bonde la Rwabushakira Wilayani Huye, anayehusika na utafutaji wa maji, anasema walianza kulima mwaka 2003, ambapo kila mmoja alilima peke yake.
Ilipofika 2006, watu walianza kuungana, ambapo watu 20 walianzisha kikundi.
Baadaye, kikundi hicho kilienda kutafuta usajili wa kisheria na kuwa Chama cha Ushirika kisha kikathibitishwa mwaka 2012. Vikundi vingine navyo vilipoona jinsi chama cha ushirika kilivyosaidia watu kujiendeleza, vikachagua kujifunza kutoka kwa wenzao.

Alisema: “Walipoona kwamba wenzao wanaendelea kupitia kujilipia Bima ya Afya (Mituel), wengine wakinunua mifugo na kuwasomesha watoto wao, ilibidi sisi sote tuwaombe waliokuwa wamebaki kuungana katika Chama cha Ushirika.”
Anaendelea kusema kuwa katika miaka mine iliyopita wameungana pamoja, na kwamba chama cha ushirika kimeshawafikisha kwenye mengi, ikiwemo kupewa mbuzi na kupewa majembe ya kutumia.
Alisema: “Katika miaka 4 iliyopita tumeungana pamoja na kimeshatufikisha kwenye mengi, ikiwa ni pamoja na kununuliwa mbuzi, na tulivyo watu 56, kila mmoja alipewa jembe, hatuna shida tena.”
Mazimpaka anasema kabla ya SAIP kuja walikuwa wakiishi maisha yasiyo mepesi, wakilima mahindi kwa kutumia mbinu za kienyeji na beseni, kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kununua mashine.
Alisema: “Tulilima mahindi lakini tukitumia njia ya kienyeji tukimwagilia kwa beseni kwa sababu hatukuwa na uwezo wa kununua mashine hizi, lakini SAIP ilitusaidia kutupeleka RAB, wakatupa zana na kutupa Faranga Milioni Moja na Laki Mbili na Arobaini (1,250,000 Frw).”
Anasema uzalishaji umeongezeka ukilinganisha na wakati walipotumia beseni. Puria walivuna kati ya tani 5 na 6, lakini sasa wamefikia kuvuna tani 16 kwenye hekta 7.
Alisema: “Katika mashine tulizopewa na SAIP zinatusaidia kwenye hekta 4 kutokana na kwamba kuna eneo maji hayapatikani kutokana na misimu.”
SAIP II Katika Shughuli za Kumwagilia Maji
SAIP II ni mradi unaolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo, kutafuta masoko na kujitosheleza kwa chakula.
SAIP I ni Second Sustainable Agricultural Intensification and Food Security Project, na ilifanya kazi katika wilaya 9, wakati awamu ya SAIP II imefanya kazi katika wilaya 20. SAIP II itamalizika Desemba 2026.
Baadhi ya shughuli ambazo mradi huu uliwekea msisitizo na zikawafaa wakulima ni kuwapa zana za kumwagilia maji katika maeneo madogo (Small Scale Irrigation Technology), zinazowawezesha kulima msimu yote, na hivyo uzalishaji kuongezeka, wakaweza kuishi vyema katika kaya zao na kupata vya kupeleka sokoni.
SAIP pia ilisaidia wakulima kwa kuwapa zana zinazowasaidia kumwagilia maji katika maeneo madogo kuanzia hekta 0.5 hadi hekta 10. Pia kuna zana zinazotumia nishati ya jua (solar-powered irrigation systems) pamoja na pampu za dizeli (Diesel pumps).
SAIP I ilisaidia wakulima kumwagilia maji kwenye zaidi ya hekta 1,367, huku SAIP II ikiwa imeshamwagilia kwenye hekta 1,200, wakati kukiwa kumepangwa hekta 1,000.
Waliosaidiwa na SAIP I na SAIP II wote pamoja ni 3,369, wakiwemo wanaume 1,916 na wanawake 1,453.
SAIP II inafanya kazi katika wilaya ishirini ambazo ni Huye, Nyagatare, Kirehe, Gatsibo, Bugesera, Kayonza, Ngoma, Rwamagana, Rusizi, Karongi, Nyabihu, Kamonyi, Muhanga, Nyanza, Gisagara, Nyamagabe, Rulindo, Ngororero, Ruhango na Rutsiro.











