Ijumaa, Julai 10, 2026
spot_imgspot_img

Top 5 This Week

spot_img

Related Posts

Rwanda hupoteza takribani tani 27 za udongo kwa kila hekta kila mwaka kutokana na mmomonyoko

Na Seif Shaggy Gracien Hasingizwimana/Kigali,Rwanda,

Katika mpango wa kukuza kilimo endelevu na kulinda udongo, Serikali ya Rwanda inawashauri wakulima kubadili mifumo ya asili ya ukulima, na badala yake watumie kilimo hifadhi kinachorudisha uhai wa udongo (Regenerative Agriculture), kwa kufunika udongo ili kupunguza mmomonyoko na kuongeza uzalishaji.

Hayo yalibainishwa na Dkt. Patrick Karangwa, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Kilimo na Mifugo (MINAGRI), ambapo alisema kuwa Serikali ya Rwanda imedhamiria kuboresha kilimo na ufugaji ili nchi ifikie uzalishaji wa kutosha wa chakula na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Alisema: “Kupitia Wizara ya Kilimo na Mifugo, Serikali ya Rwanda imedhamiria kubadili kilimo na ufugaji wa asili ili nchi yetu ifikie uzalishaji wa kutosha wa chakula na pia kutoa mchango katika maendeleo ya kiuchumi. Lengo letu ni kuboresha kilimo kwa njia endelevu.”

Dkt. Karangwa anawataka wakulima kupokea mifumo mipya ya ukulima, wachee kulima udongo wote kama ilivyokuwa ikifanyika awali, bali watumie mfumo wa kilimo kinachorudisha uhai wa udongo.

Alisema: “Tunawahimiza wakulima kubadili jinsi wanavyolima udongo wao kwa kufanya kilimo cha kisasa ambacho si cha kulima shamba lote. Badala yake, mkulima anapaswa kuandaa tu pale mbegu na mbolea zinapowekwa. Kulima udongo wote kunaharakisha mmomonyoko, na takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Rwanda hupoteza takribani tani 27 za udongo kwa kila hekta kila mwaka kutokana na mmomonyoko.”

Alisisitiza kuwa kulinda udongo ndiyo nguzo ya maendeleo ya kilimo endelevu, akisema kuwa kilimo kinachorudisha uhai wa udongo (Regenerative Agriculture) kinatoa majawabu madhubuti ikiwa ni pamoja na kupunguza mmomonyoko, kulinda viumbe hai vilivyopo chini ya udongo, kurudisha rutuba ya udongo, kuongeza uzalishaji kwa muda mrefu na kukuza matumizi ya teknolojia inayotumia nishati mbadala inayosaidia kupunguza gesi chafu na kuongeza uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima pia wanahimizwa kujiunga katika vyama vya ushirika (ushirika) na kushirikiana ujuzi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazopelekwa sokoni.

Hii ni huku Rwanda ikiendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupungua kwa rutuba ya udongo pamoja na kupanda kwa bei za mazao yatokanayo na kilimo na ufugaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Popular Articles