Na Seif Shaggy Gracien Hasingizwimana/Kigali,Rwanda
Gatsibo- Uzalishaji wa maziwa katika Wilaya ya Gatsibo umeongezeka kwa lita 15,000 kwa siku katika miaka miwili iliyopita, ukipanda kutoka lita 45,000 hadi kufikia lita 60,000 kwa siku, huku wilaya hiyo ikiwa na lengo la kufikia lita 100,000 kwa siku katika miaka ijayo.
Ongezeko hili linahusiana na utekelezaji wa Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Maziwa nchini Rwanda Awamu ya Pili (RDDP II), ambao unawasaidia wafugaji kuongeza uzalishaji kupitia uendelezaji wa nyasi za mifugo na kuwapa mafunzo ya ufugaji wa kisasa.
Ismael Ngendahayo, mkulima wa nyasi na mbegu zake katika Kijiji cha Akabuga, Kata ya Kiramuruzi, ni mmoja wa wale ambao tayari wameona mabadiliko yatokanayo na kulima nyasi za kisasa za mifugo.

Alisema: “Kupitia msaada wa RDDP II, niligundua kuwa kutegemea aina moja tu ya nyasi hakuwezi kumpa ng’ombe virutubisho vyote anavyohitaji. Kama walivyo binadamu, ng’ombe nao wanahitaji mlo kamili wenye virutubisho vinavyotia nguvu na vile vinavyojenga mwili.”
Ngendahayo anasema kuwa alianza kwenye eneo dogo la mita 20 kwa 20, lakini kwa sasa amefikia hekta mbili za nyasi za kisasa. Anasema pia kwamba katika msimu mmoja alipata pesa za Rwanda takriban milioni mbili kutokana na kuuza mbegu za nyasi.
Alisema: “Pesa hizo nilizitumia kununua ng’ombe mwenye thamani ya faranga za Rwanda milioni moja, na zilizobaki nikaziwekeza katika kuendeleza mashamba na kununua mbolea.”
Anasema kuwa uzalishaji wa maziwa umeongezeka sana kwa sababu hapo awali ng’ombe wake walikuwa wanatoa lita moja kwa siku, wakati sasa kuna wanaozidi lita 10 kwa siku.
Alisema: “Zamani nilikuwa nawalisha zaidi vyakula vya kutia nguvu. Sasa ninavichanganya na nyasi zenye protini nyingi na kufuata taratibu za ulishaji tulizofundishwa. Tofauti ni kubwa sana.”
Peter Muyambe, anayefuga katika Kijiji cha Rwiminazi, Kitongoji cha Nyamatete, Kata ya Rwimbogo, anasema kuwa kulima nyasi za mifugo kumebadilisha sana ufugaji wake.

Alisema: “Nyasi za kisasa zinatoa mazao mengi zaidi kuliko kutegemea malisho ya asili pekee. Zinaweza kuvunwa mara nne kwa mwaka.”
Muyambe anasema kuwa kabla ya kufundishwa kilimo cha nyasi, ng’ombe wao walikuwa wanatoa lita moja au mbili kwa siku, lakini sasa kuna wanaotoa hadi lita 15 kwa siku.
Alisema: “Kabla ya kujua jinsi ya kulima nyasi, ng’ombe wetu walikuwa wanatoa lita moja au mbili za maziwa kwa siku. Sasa kuna wanaotoa hadi lita 15.”
Anaendelea kusema kuwa tatizo la upungufu wa chakula cha mifugo wakati wa kiangazi limepungua kwa kiasi kikubwa.
Alisema: “Kuanzia mwezi Mei hadi Oktoba tulikuwa hatuwezi kukua ng’ombe wetu kwa sababu hakukuwa na nyasi. Sasa tatizo hilo linapungua kwa sababu tuna nyasi za kutosha kulingana na idadi ya wanyama ambao mtu anao.”
Kwa upande wa uongozi wa Wilaya, Makamu wa Meya wa Wilaya ya Gatsibo anayehusika na Maendeleo ya Kiuchumi, Jean Leonard Sekanyange, anasema kuwa RDDP II inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza ufugaji wa maziwa.

Alisema: “Mradi huo umesaidia wananchi wetu kwa kutoa ng’ombe wa kisasa na kuendeleza kilimo cha nyasi za mifugo.”
Aliendelea kusema kuwa tatizo la uhaba wa chakula cha mifugo lilikuwa kubwa, lakini wafugaji na wazalishaji wa mbegu za nyasi wanasaidiwa kuongeza uzalishaji.
Alisema: “Zamani tatizo la uhaba wa chakula cha mifugo lilikuwa kubwa. Kupitia RDDP II, wafugaji na wazalishaji wa mbegu za nyasi wanasaidiwa kulima nyasi ili kupatikane chakula bora cha mifugo, na hivyo uzalishaji wa maziwa uongezeke.”
Wilaya ya Gatsibo imeshafikia uzalishaji wa lita 60,000 za maziwa kwa siku kutoka lita 45,000 katika miaka miwili iliyopita, na ina lengo ambalo ni kufikia lita 100,000 kwa siku katika miaka ijayo.
RDDP II ni mradi utakaodumu kwa miaka sita kuanzia mwaka 2024 hadi 2030, ukiwa na bajeti ya dola za Kimarekani milioni 100.37 (zaidi ya faranga za Rwanda bilioni 127). Utatekelezwa katika wilaya 27 za nchi na unatarajia kufikia kaya 175,000, ambazo ni sawa na wananchi takriban 700,000.








