Na Seif Shaggy Gracien Hasingizwimana
Timu ya Rayon Sports imekata tiketi ya kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Amani la mwaka wa 2026, baada ya kutoka sare ya 0-0 na Gorilla FC katika mechi ya marudiano iliyopigwa Jumanne hii kwenye Uwanja wa Kigali Pele Stadium.
Licha ya mechi hii ya marudiano kumalizika kwa timu zote mbili kutoka sare ya bila kufungana, Rayon Sports imesonga mbele kutokana na bao la ugenini ililopata katika mechi ya kwanza, ambapo timu hizo mbili zilikuwa zimetoka sare ya bao 1-1. Bao hilo ambalo Rayon Sports ililipata katika mechi iliyokuwa ugenini dhidi ya Gorilla FC, ndilo lililotumika kama kigezo cha kuwapa nafasi ya kusonga mbele kwa hesabu ya jumla ya mechi zote mbili.
Katika mechi hiyo ya marudiano, timu zote mbili zilionyesha umakini mkubwa wa kulindana katikati ya uwanja, jambo lililosababisha kutokea kwa makosa mengi ya uchezaji. Gorilla FC ilijaribu kutafuta bao kupitia nafasi ilizopata katika dakika ya 10 kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Mosengo Tansele, pamoja na shuti kali la Ndikumana Asman, lakini Nshimiyimana Emmanuel ‘Kabange’ alicheza vizuri katika safu ya ulinzi ya Rayon Sports na kuondoa mipira hiyo iliyoweza kuzaa mabao.

Katika kipindi cha pili, Rayon Sports ndiyo ilitawala mpira zaidi ikitafuta mbinu za kushambulia, lakini mechi ilimalizika huku timu zote zikiwa zimetoka sare ya 0-0. Katika harakati za kutafuta matokeo, makocha wa timu zote mbili walifanya mabadiliko ambapo kwa upande wa Gorilla FC waliingia Chancelor Ndong Mengue na Karenzo Alexis, huku Rayon Sports ikimtoa Mugisha Didier na kumwingiza Sindi Paul Jesus.
Rayon Sports sasa inasubiri kujua timu itakayokutana nayo kati ya mpinzani wake APR FC na Etincelles FC katika mechi ya marudiano, ambapo inatarajiwa kufanyika Jumatano hii tarehe 13/05/2026 saa 18h00′.
APR FC ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kukutana na Rayon Sports ikizingatiwa kuwa katika mechi ya kwanza ilikuwa imeshinda mabao 3-1.







