Na Seif Shaggy Gracien Hasingizwimana/Kigali,Rwanda,
Seneta Mukabalisa Donatille, aliyekuwa Rais wa Baraza la Wawakilishi (Spika), amefariki dunia kutokana na ugonjwa uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu. Amefariki katika Hospitali ya King Faisal ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa kutoka Igihe zinasema kuwa kifo chake kimejulikana asubuhi ya leo Alhamisi, tarehe 30/07/2026. Mmoja wa Maseneta waliofanya naye kazi aliiambia Igihe kuwa alitembelea hospitalini hivi karibuni ambako alikuwa akitibiwa.
Mukabalisa Donatille alizaliwa Nyamata katika Wilaya ya Bugesera mnamo Julai 1960. Alikuwa mwalimu wa sheria katika Chuo Kikuu Huru cha Kigali (ULK), na pia alifanya kazi katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikijumuisha Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Maendeleo (UNDP) kwa kipindi cha miaka 16.
Mnamo Oktoba 2003, Mukabalisa alichaguliwa kuwa Mbunge, nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 2008. Baadaye alikuwa Seneta kutoka mwaka 2011 hadi 2013, kabla ya kurejea katika Baraza la Wawakilishi mwaka 2013, ambapo aliongoza hadi mwaka 2024.
Hakugombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2024 baada ya kumaliza muhula miwili katika baraza hilo.
Pia, Mukabalisa Donatille alikuwa Rais wa chama cha Liberal Party (PL), kilichoanzishwa tarehe 14 Julai 1991.





